Friday, June 17, 2016

MKUTANO WA SITINI NA NANE WA KAMATI KUU YA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO-EXCECUTIVE COUNCIL-68), GENEVA, USWISI, TAREHE 15-24 JUNI, 2016



Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa,Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Mjumbe wa “WMO Excecutive Council” na Bw. Wilbert Timiza Muruke, Meneja Mahusiano ya Kimataifa wa TMA katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa Kamati Kuu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO-Excecutive Council-68) unaondelea, Geneva, Uswisi kuanzia tarehe 15-24 Juni 2016.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi alikuwa miongoni mwa wajumbe 37 wa Mkutano wa Sitini na Nane wa Kamati Kuu ya Utendaji ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization Executive Council WMO-EC 68) unaofanyika makao makuu ya Shirika hilo, Geneva nchini Uswisi kuanzia tarehe 15 hadi 24 Juni, 2016. Pia Dkt. Kijazi anaingia katika Kamati Kuu ya WMO akiwa kati ya wanawake wawili (2) kutoka Afrika na watano (5) kati ya thelathini na saba (37) kuwakilisha Dunia nzima.
Mkutano wa WMO-EC-68 pamoja na masuala mengine unajadili masuala mbalimbali ya uboreshaji wa huduma za hali ya hewa Duniani sambamba na kutimiza Makubaliano ya Kikanda na Kimataifa katika kukabiliana na athari zinazosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.
Aidha masuala yanayojadiliwa ni sehemu ya Mpango Mkakati wa WMO na vipaumbele vyake katika kipindi cha mwaka 2015-2019 unaojumuisha utekelezaji wa programu za utoaji wa huduma bora zaidi za hali ya hewa kwa jamii “Global Framework for Climate Services”, Utekelezaji wa programu ya uboreshaji wa vituo vya upimaji wa hali ya hewa na ubadilishanaji wa data za hali ya hewa “WMO Integrated Global Observing System and Information System (WIGOS/WIS), utoaji wa tahadhari za mapema ili kukabiliana na maafa “Disaster Risk Reduction, Resilience and Prevention”, Uboreshaji wa huduma za usalama na usafiri wa anga “Aviation meteorological services”, Kuboresha huduma za hali ya hewa kwa maeneo ya Dunia yenye barafu ya asili ikiwa ni pamoja na milima mirefu kama Kilimanjaro “Polar and high mountain regions”, Kujenga uwezo wa rasilimali watu na vitendea kazi hasa kwa nchi zinazoendelea na visiwa vidogo na tafiti za hali ya hewa. Aidha Mkutano huu unajadili pia namna ya kushirikiana na mashirika mengine ya kimataifa kama njia ya kuboresha huduma za hali ya hewa kote duniani na kutatua changamoto za athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi na uhifadhi wa mazingira.
IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI-AFISA UHUSIANO TMA


No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...