Sunday, April 24, 2016

BODI YA USHAURI YA MAMLAKA YA HALI YA HEWA YASISITIZA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU KWA KUZINGATIA MAADILI, KANUNI NA TARATIBU ZA KAZI KWA WATUMISHI WA MAMLAKA YA HALI YA HEWA






Katika jitihada za kuhakikisha Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inafikia viwango vya kimataifa kulingana na matakwa ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma kimefanikiwa kufanya awamu ya tatu ya  kozi ya huduma za hali ya hewa kwa usafiri wa anga kwa baadhi ya wafanyakazi wa TMA.

Akifunga rasmi kozi hiyo na kuwatunuku vyeti wahitimu, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi aliwataka wahitimu wote pamoja na wafanyakazi wengine wa Mamlaka kuwa vielelezo katika vituo vyao vya kazi katika kuzingatia maadili, kanuni na taratibu za kazi na kufanya kazi kwa weledi mkubwa hususani kwenye sekta ya usafiri wa anga. Aidha aliahidi kwamba Bodi itashirikiana na menejimenti ya TMA kuhakikisha kwamba miundo mbinu ya Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma inaboreshwa.

Akimkaribisha mgeni rasmi Dkt. Agnes Kijazi, Mkuruggenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa alisema mafunzo hayo ni sehemu ya kutekeleza mpango mkakati wa Mamlaka wa kuendeleza watumishi ili kukidhi viwango vya Shirika la Hali ya Hewa Duniani.

Naye Mkuu wa Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma, Bw. Joseph Aliba alitoa shukrani za dhati kwa serikali kwa kuwezesha uboreshaji wa huduma kama vile usajili wa chuo, maktaba, ujenzi wa uzio wa chuo, mafunzo kwa waalimu, kuunganishwa katika mkongo wa Taifa huku akitaja baadhi ya changamoto zilizopo.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wote, Bi. Beatrice Kitero, alishukuru Mamlaka kwa mafunzo na kuahidi kuyafanyia kazi katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa kwaajili ya usafiri wa anga nchini.

Kozi ya huduma za hali ya hewa kwaajili ya usafiri wa anga, imeandaliwa na Chuo cha Hali ya Hewa  Kigoma kwa muda wa mwezi mmoja na ilifanyika Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza, Dar es Salaam. Wahitimu ni wafanyakazi wa Mamlaka waliohitimu degree ya Hali ya Hewa kutoka vituo vya Mbeya, Dodoma, Kigoma, Makao Makuu (DSM) na Zanzibar.



No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...