Tuesday, September 1, 2015

WANAHABARI WAPATA MAFUNZO YA EL-NINO NA MCHANGO WAKE KATIKA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA VULI 2015.



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi amekutana na baadhi ya wanahabari kutoka vyombo mbali mbali vya habari nchini katika warsha ya siku moja iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ubungo Plaza Dar es Salaam tarehe 01 Septemba 2015.

Katika warsha hiyo Dkt. Kijazi aliwaasa wanahabari kuhusiana na lugha inayotumika sambamba na elimu ya kina kuhusiana na EL-NINO. ‘Tunatambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari nchini hivyo Mamlaka imeandaa warsha hii tukiwa na nia ya kupata na kutoa mrejesho wa lugha gani itumike ili kuwarahisishia wanahabari na jamii kwa ujumla kuelewa taarifa za hali ya hewa hususani suala la El Nino’ alisema Dkt. Kijazi

Aidha mtaalamu Bw. Samuel Mbuya Kutoka TMA alifananua kuhusiana na namna El Nino inavyotokea na sababu zake kwa kuzungumzia ongezeko la joto katika Bahari ya Pasifiki hivyo kuchangia kubadilisha mifumo ya hali ya hewa kwa dunia nzima.

Kwa upande wa wanahabari, Bi. Grace Kingalame kutoka TBC1 alisema ‘Semina ni hii inatusaidia wanahabari kujifunza vitu vingi kuhusiana na hali ya hewa jambo ambalo linatupa uwanja mpana wa kuandika habari zinazohusu masuala ya hali ya hewa kwa usahihi zaidi na hata kuwafikia wananchi tukiwa na taarifa zilizo sahihi kama vile tahadhari za majanga yanayosababishwa na mvua au mabadiliko ya tabia nchi. Hivyo ni vyema Mamlaka ikaendelea kutoa mafunzo haya mara kwa mara kwa ili kuweka mazingira mazuri ya taarifa zake kuripotiwa kwa usahihi’Alisema Grace.

TMA imekuwa ikiandaa warsha mbalimbali kwa wadau mbalimbali wakiwemo wanahabari katika mwendelezo wa utoaji elimu ya sayansi ya hali ya hewa pamoja na kudumisha ushirikiano baina ya Mamlaka na watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ambao ni wadau kutoka sekta mbalimbali.

Akifungua warsha hiyo Dkt. Kijazi alisema Mamlaka itatoa mwelekeo wa mvua za Vuli kesho tarehe 2 Septemba 2015 saa tano asubuhi.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dk.Kijazi akisalimiana na wanahabari katika warsha iliyofanyika
Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dk.Kijazi akisalimiana na wanahabari katika warsha iliyofanyika
Wanahabari wakiendelea na warsha katika ukumbi wa mikutano wa TMA-Makao Makuu tarehe 01 Septemba 2015



IMETOLEWA NA MONICA MUTONI; AFISA UHUSIANO, MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.



No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...