Thursday, June 18, 2015

KIKAO CHA KIKOSI KAZI CHA “AFRICAN MINISTERIAL CONFERENCE ON METEOROLOGY (AMCOMET) TECHNICAL TASK FORCE ON AFRICAN REGIONAL SPACE PROGRAMME ON METEOROLOGY” KILICHOFANYIKA GENEVA, USWISI, TAREHE 10 JUNI 2015



Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (akiwakilisha Tanzania) katika picha ya pamoja na washiriki wa kikosi kazi cha “African Ministerial Conference on Meteorology (AMCOMET) Technical Task Force on African Regional Space Programme on Meteorology” Geneva, Uswisi tarehe 10 juni 2015.


Tanzania ambayo ni mwenyekiti wa kikosi kazi cha “African Ministerial Conference on Meteorology (AMCOMET) Technical Task Force on African Regional Space Programme on Meteorology” iliongoza kikao cha kikosi kazi hicho kilichofanyika tarehe 10 Juni 2015 sambamba na Mkutano Mkuu wa 17 wa Shrikika la Hali Duniani (WMO-CONGRESS-17)  huko Geneva nchini Uswisi. Kikao kiliendeshwa chini ya Dkt. Agnes Kijazi kwa mafanikio makubwa.
Mkutano huo wa kikosi kazi ulifanyika kwa kutumia fursa ya kuwepo washiriki katika Mkutano Mkuu wa 17 wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO Congress-17).  Lengo la mkutano lilikuwa kubadilishana uzoefu na nchi ambazo zimepiga hatua katika masuala ya hali ya hewa katika anga za juu (Space Meteorology). Aidha kikao pia kilijadili upatikanaji wa vyanzo vya mapato ambavyo vitasaidia kufanikisha programu hii na miradi itakayofanyika wakati wa utekelezaji wa program hii. 

Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ambaye pia ni mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na mwenyekiti wa mkutano huo akiendesha Mkutano wa Kamati ya Kikosi Kazi cha Programu ya anga za juu ya AMCOMET, Geneva, Uswisi. Kulia kwake ni Dkt. Joseph Kanyanga kutoka Zambia akiwakilisha AMCOMET Bureau na Dkt. Amosi Makarau, Rais wa RA1; Kushoto kwake ni wawakilishi wawili wa Sekretarieti ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO Secretariat).  
Katika ufunguzi wa mkutano huo, Dkt. Agnes Kijazi alirejea kwa kifupi makubaliano yaliyofanyika katika mkutano wa tatu wa Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya hali ya hewa Afrika (AMCOMET) uliofanyika huko Praia, Cabo Verde, ambapo kikosi kazi kiliongezewa jukumu la kuendelea na upembuzi yakinifu wa mpango mkakati wa utekelezaji wa programu ya hali ya hewa ya anga za juu barani Afrika. Dkt. Kijazi aliongezea kusema kuwa kikosi kazi kupitia mwenyekiti Tanzania kilishiriki kikamilifu katika kuandaa rasimu za sera na mpango mkakati wa anga za juu wa Umoja wa Afrika (Space Policy and Implementation Plan). Ushiriki huu ulihakikisha kuwa masuala ya hali ya hewa yanaingizwa katika rasimu hizi. Pia alifahamisha kikao kuwa mkutano wa tatu (3) wa Mawaziri uliofanyika Cabo Verde ulipitisha rasimu hizo. Aidha Dkt. Kijazi aliwashukuru wajumbe wa kikosi kazi hiki kwa kuiamini Tanzania kuwa Mwenyekiti wake.  Kwa upande wake Dr. Joseph Kanyanga (Zambia) kama mwakilishi wa ‘AMCOMET Bureau’ alisema makubaliano ya kikao hicho yatajadiliwa katika kikao kijacho cha Bureau. Dr. Amosi Makarau (Zimbabwe) ambaye ni Rais wa Africa katika masuala ya hali ya hewa alikishukuru kikosi kazi kwa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa majukumu yake.


Katika kikao hicho baadhi ya mashirika na nchi zilizopiga hatua katika eneo la teknonojia ya anga za juu ziliwasilisha mada zenye lengo la kubadilishana uzoefu. Nchi hizo ni China, Nigeria, Afika ya Kusini pamoja na Taasisi ya Umoja wa Ulaya ya “European Meteorological Satellite Agency (EUMETSAT)” na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO). WMO waliwasilisha mada kuonyesha hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa program hii.
Mkutano ulikuwa na maazimio  kadhaa ikiwa ni pamoja na kuharakisha utekelezaji wa program hiyo ya anga za juu. Kuboresha rasimu ya utekelezaji inayoandaliwa kwa kujumuisha uzoefu wanchi zilizowasilisha mada katika kikao hicho. Aidha suala la kujengewa uwezo (capacity Building) lilionekana kuwa la muhimu hasa katika kuamua hatua ya kuanza kutekeleza program hiyo kati ya hatua tatu zilizoainishwa ambazo ni “Ground Segment, Application Segment and Space segment”

Kikosi kazi cha program ya Anga za juu cha AMCOMET (AMCOMET task force on African Meteorological Space Programme) kinaundwa na Tanzania (Mwenyekiti), Afrika ya Kusini (Rapporteur), Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nigeria na Algeria.
IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI-AFISA MAHUSIANO TMA






No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...